Sunday, March 20, 2011

NINI KIFANYIKE KWA TATIZO LISILOKWISHA LA WANAUME WANAONYANYASA WANAWAKE KIJINSIA?

TATIZO LA UNYANYASAJI KIJINSIA: NINI DAWA YAKE?
Je, umefika sasa Wanawake waanze kuwachapa viboko na miiko wanaume wanaowanyanyasa kijinsia kama anavyofanya mama huyu hapa chini?

Tatizo hili limekuwepo katika jamii yetu miaka nenda miaka rudi na halionekani kukoma leo. Sera na Sheria nyingi zimetungwa kukabiliana nalo. Tafiti lukuki zimefanywa. Makongamano, Semina na warsha zisizoisha zimefanyika katika kuelimishana na kutafuta dawa ya tatizo hili la udhalilishaji na unyanyasaji ki-jinsia lakini bado halikomi.


Sisi Wabunge, kama walivyo Wawakilishi, wanaharakati na wapenda haki na usawa wengine tungeomba tupatiwe mawazo mbalimbali kutoka kila mmoja ndani ya jamii yetu na mwingine yeyote aliyestaaribika na katika kutafuta tiba ya kudumu na isiyo na ubabaishaji kukabiliana na usugu wa tatizo hili. Swali la Msingi ambalo halijapata jibu la kutosha ni hili: NINI KINAPASWA KUFANYIKA?; Je Wanaume na wote wanaonyanyasa wanawake na watoto kijinsia wachapwe viboko?, majina yao yatangazwe kwenye vyombo vya habari; Watengwe?. Yote yanahitaji mchango wetu wote. Kuna jamii katika historia ziliwahasi wabakaji. Kuna nchi kama Marekani wale wanaopatikana na makosa ya ubakaji wanawekwa katika mfumo maalum wa ki-kompyuta [Sexual Offenders Database] ambao kila mtu katika jamii anaweza kuwatambua na kuwaona majina yao. Wengine wanazuiliwa wasitoke mahali walipo bila idhini maalum au kupigwa marufuku kuwa karibu na akina mama au watoto. Tuelekee huko?

Tunahitaji maoni na mchango wa kila mmoja wetu. Hili si suala tu la Wabunge, Wahanga, vyombo vya habari, wanasiasa au Taasisi fulani fulani za masuala ya kijinsia ni letu wote. Ni tatizo linalomuathiri kila mmoja wetu-watoto wetu, mama zetu, dada zetu, majirani zetu na kikubwa, Watanzania na binadamu wenzetu wanaostahili kulindwa na kutetewa utu na haki zao za msingi. Ile kasumba ya kizamani kuwa 'jambo hili halihusu' ni ya kuifikiria mara mbili mbili maana walioathiriwa leo na mambo haya hawakuwa wanafahamu jana yake kama yangewatokea wao au ndugu zao. Tunahitaji mchango wetu sote.

No comments:

Post a Comment