Sunday, March 20, 2011

WATANZANIA NA HASA AKINA MAMA TUNAHITAJI KUJIELIMISHA KILA KUKICHA KAMA NAMNA YA MAANA ZAIDI KUJIKOMBOA

Ukombozi wa Mtanzania, na hasa Mwanamke unahitaji sana uelewa wake katika kile kinachoendelea nchini na kote duniani. Na hili (yaani uelewa mdogo au usioridhisha) ndilo kikwazi kikubwa katika harakati za kumkomboa mwanamke nchini. Kifupi tu ni kuwa ni vigumu sana kupigania haki yako kama huifahamu haki hiyo ni ipi, mevunjwa katika mazingira gani au ni hatua zipi na wapi unaopaswa kwenda inapokiukwa.


Ki-msingi basi ni vema tukumbushane tena na tena kuwa Mbunge, NGO au vyombo vya habari tu peke yao haviwezi kuleta mabadaliko makubwa zaidi katika ukombozi wa mwanamke ukilinganisha na ukombozi wake ki-fikra kwanza. Uelewa wake katika haki za msingi za binadamu, sheria za nchi, sera za Taifa, kumbukumbu ya ahadi zilizotolewa kabla na serikali/vyama vya siasa na utekelezaji wa ahadi hizo, maamuzi ya mahakama, mikataba ya kimataifa kuhusu ulindwaji na utekelezaji wa haki za msingi za wanawake, watoto na ki-jinsia ni mambo yenye umuhimu mkubwa na wa pekee kuanza nayo sasa.


Yote haya yako katika makabrasha ila watu wanaohitaji kuyajua hawayafahamu vizuri. Tufanye nini zaidi ya kile kilichofanyika sasa? Tubadilishane mawazo kama tunahitaji kubadilisha tena sheria kama sheria ya ndoa ili kila anayeomba na kupewa hati ya ndoa apewe pia elimu na nyaraka zilizotajwa hapo. Au mambo haya yapew msukumo kama izungumzwavyo elimu ya kupiga kura? Au tubadili mitaala (curricula/syllabuses) zetu ili kila Mwanafunzi alazimishwe kusoma elimu ya jinsia kama ilivyokuwa kwa somo la Siasa na Civic (Uraia) Mashuleni?; Ama makampuni yalazimshwe kutumia kiasi fulani cha bajeti zao katika kufanikisha Wajibu Wao wa Kijamii (Corporate Social Responsibilities)?

NINI KIFANYIKE KWA TATIZO LISILOKWISHA LA WANAUME WANAONYANYASA WANAWAKE KIJINSIA?

TATIZO LA UNYANYASAJI KIJINSIA: NINI DAWA YAKE?
Je, umefika sasa Wanawake waanze kuwachapa viboko na miiko wanaume wanaowanyanyasa kijinsia kama anavyofanya mama huyu hapa chini?

Tatizo hili limekuwepo katika jamii yetu miaka nenda miaka rudi na halionekani kukoma leo. Sera na Sheria nyingi zimetungwa kukabiliana nalo. Tafiti lukuki zimefanywa. Makongamano, Semina na warsha zisizoisha zimefanyika katika kuelimishana na kutafuta dawa ya tatizo hili la udhalilishaji na unyanyasaji ki-jinsia lakini bado halikomi.


Sisi Wabunge, kama walivyo Wawakilishi, wanaharakati na wapenda haki na usawa wengine tungeomba tupatiwe mawazo mbalimbali kutoka kila mmoja ndani ya jamii yetu na mwingine yeyote aliyestaaribika na katika kutafuta tiba ya kudumu na isiyo na ubabaishaji kukabiliana na usugu wa tatizo hili. Swali la Msingi ambalo halijapata jibu la kutosha ni hili: NINI KINAPASWA KUFANYIKA?; Je Wanaume na wote wanaonyanyasa wanawake na watoto kijinsia wachapwe viboko?, majina yao yatangazwe kwenye vyombo vya habari; Watengwe?. Yote yanahitaji mchango wetu wote. Kuna jamii katika historia ziliwahasi wabakaji. Kuna nchi kama Marekani wale wanaopatikana na makosa ya ubakaji wanawekwa katika mfumo maalum wa ki-kompyuta [Sexual Offenders Database] ambao kila mtu katika jamii anaweza kuwatambua na kuwaona majina yao. Wengine wanazuiliwa wasitoke mahali walipo bila idhini maalum au kupigwa marufuku kuwa karibu na akina mama au watoto. Tuelekee huko?

Tunahitaji maoni na mchango wa kila mmoja wetu. Hili si suala tu la Wabunge, Wahanga, vyombo vya habari, wanasiasa au Taasisi fulani fulani za masuala ya kijinsia ni letu wote. Ni tatizo linalomuathiri kila mmoja wetu-watoto wetu, mama zetu, dada zetu, majirani zetu na kikubwa, Watanzania na binadamu wenzetu wanaostahili kulindwa na kutetewa utu na haki zao za msingi. Ile kasumba ya kizamani kuwa 'jambo hili halihusu' ni ya kuifikiria mara mbili mbili maana walioathiriwa leo na mambo haya hawakuwa wanafahamu jana yake kama yangewatokea wao au ndugu zao. Tunahitaji mchango wetu sote.

Saturday, March 12, 2011

MATATIZO MAKUU YA MSINGI YANAYOMKABLI MWANAMKE WA KITANZANIA

MATATIZO MAKUU YA MSINGI YANAYOMKABLI MWANAMKE WA KITANZANIA

MAAMUZI MUHIMU YA MAHAKAMA KUHUSIANA NA HAKI ZA MWANAMKE TANZANIA

MAAMUZI MUHIMU YA MAHAKAMA KUHUSIANA NA HAKI ZA MWANAMKE TANZANIA

Mahakama zetu Kikatiba zimepewa jukumu la kutoa haki. Akina mama ambao ni waathirika wakubwa katika masuala ya ksiheria huiona mahakama kma akimbilio la mwisho kudai haki zao. Ni vema basi tukawa karibu katiika kuyajadili maamuzi muhimu ya mahakam Kuu na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kwa sababu ndiyo hutoa msimamo kuhusu tafsiri ya Sheria fulani ambazo sisi Wabunge huzitunga mnapotupeleka Bungeni.

Hapa tutakuwa tukiyamaamuzi muhimu ya Mahakama zetuu ili tuone pia kama tunaweza kushauri yarekebishwe au yaendelezwe kumlinda mwanamke, mtoto na jamiii nzima.

SHERIA ZA TANZANIA ZINAZOMGUSA ZAIDI MWANAMKE MOJA KWA MOJA

SHERIA ZA TANZANIA ZINAZOMGUSA ZAIDI MWANAMKE MOJA KWA MOJA

Ni vema kila mwanamke wa tanzania akazifahamu au kuelimishwa kuhusu Sheria hzi ambazo zinatugusa zaidi akina mama na watoto. Tutakuwa tukizijadili kila tupatapo fursa.

1. Katiba ya Nchi ya mwaka 1977 (akama ilivyorekebishwa mara kwa mara)
2. Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971.
3. Sheria za Ardhi (namba 4 na 5) za Mwaka 1999.
4. Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Makosa ya Jinai) (Penal Code)
5. Sheria za Kazi.
6. Sheria za Kimila.
7. Sheria ya Mahakama ya 1984 (MCA)


Niaendelea na nyinginezo.

TAASISI ZINAZOHUSIKA NA MASUALA YA WANAWAKE NA JINSIA TANZANIA

TAASISI ZINAZOHUSIKA NA MASUALA YA WANAWAKE NA JINSIA TANZANIA

Friday, March 11, 2011

SALAAM ZA MBUNGE LETICIA NYERERE KWA WATANZANIA WOTE, HUSUSAN WANAWAKE

SALAAM ZA MBUNGE LETICIA NYERERE KWA WATANZANIA NA HUSUSAN AKINA MAMA WOTE

Naomba nitumie fursa hii kuwasalimia Watanzania wote, na hususan akina mama ambao katika kuadhimisha siku ya Wanawake duniani ndipo nimehamasika zaidi kufungua blogu hii kama namna ya kutekeleza uwajibikaji kwa vitendo kwa sisi Wawakilishi wenu mliotuamini na kutupa ridhaa ya kuwazungumzia matatizo yenu na yale ya Taifa zima kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania ambalo nimeingia kupitia Viti Maalum.

Ni kweli kwamba asilimia kubwa ya akina mama na hasa wale wenye matatizo makubwa katika jamii yetu, mijini na vijijini, hawana uwezo na maarifa ya kutumia teknolojia ya Habari na mawasiliano (TEKNOHAMA) kama hapa katika mtandao wa internet. Hata hivi, hili halituzuii sisi wawakilishi wenu kutumia kila mwanya wa mawasiliano yaliyopo kuwafikia zaidi wananchi na wananchi wenyewe kutufikia sisi. Na hata wachache wanaoweza kuingia na kusoma haya wana nafasi kubwa katika kuwasaidia wenzetu kwa kuwasogezea taarifa au changamoto zilizopo hapa kwa vile wote tunaishi katika nchi moja kama familia, aidha kama ni majirani, tunakutana mahali pa kazi, mikusanyiko ya hadhara na kadhalika.

Blogu hii ina mantiki pia kwa sababu inaweza kutumika kama daraja la kuwaunganisha akina mama wa Tanzania waliko kila kona ya dunia ili kujua kinachoendelea katika nchi yao na wao waweze kutoa mchango wa hali na mali katika kumkomboa mwanamke kutoka katika kitanzi cha kunyanyaswa na kufanyiwa kila namna ya ukandamizaji.

Nakusudia tusaidiane katika hili ili kuyafanya mapambano ya kuleta usawa wa kijinsia kuwa ni ya wote. Kuna dhana nyingi potofu ambazo tukiondokana nazo basi mwanamke atakombolewa. Na mwanamke akikombolewa jamii nzima inanufaika kama uzoefu na pia tofauti za kisomi zilivyothibitisha kote duniani. Na ile dhana kwamba wanawake na wanaume ni kama maadui katika harakati za kijinsia tuondokane nazo. Ni kweli kuwa ukandamizwaji uliokithiri wa wanawake hufanywa na wanaume, uondokanaji wa jambo hili ni lazima uhusishe wanawake na wanaume wote-yaani jamii nzima. Na hili linathibitishwa na ukweli kwamba wapo wanaume waliosaidia sana kumkomboa mwanamke kote duniani na hata Tanzania. Waasisi wa taifa letu, hayati Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Sheikh Abeid Amani Karume na wale waliowafuata walihusika katika hili. Mahakama zetu zimesaidia mno kama inayodhirishwa na maamuzi mengi ya Mahakama za Tanzania kama yalivyotolewa na Majaji kama akina Jaji Mwalusanya na maamuzi kadhaa ya msingi yaliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, ikiwemo hukumu ya Mahakama ya Rufaa ya mwaka 1983 (Bi.Hawa Sefu Dhidi ya Ally Mohammed) ambapo mahakama zetu zilitambua kwa dhati nafasi hata ya mama wa nyumbani katika kuleta ustawi wa familia. Bunge letu limesaidia pia kama ilivyothibitishwa kwa sheria zilizoondokana ana ukandamizwaji wa maslahi ya mwanamke kama vile Sheria za Ardhi za 1999 (Sheria na 4 na Sheria na 5), marekebisho katika Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na kutungwa kwa Sheria ya makosa kama Kubaka na yanayofanana nayo. Taasisi na Mashirika ya Kiserikali kama TAMWA, TGNP, TAWLA, WLAC, HAKIELIMU, HAKIARDHI na mengineyo yametusaidia sana wanawake wa Tanzania. Vyombo vya habari pia vimefanya kazi kubwa.

Nimalize kwa kuisema kwamba Katiba ya nchi inampa fursa kila Mtanzania kushiriki katika masuala ya kitaifa ikiwemo kujua na kuishiriki katika kile ambacho Serikali inakifanya. Basi kuanzia sasa ni vema tukalizingatia hili na tusisite kushirikishana katika kuifikia serikali (Wizara, Idara za Serikali, Mashirika ya Umma, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Halmashauri zetu katika Serikali za Mitaa na kila taasisi au chombo cha kiserikali). Hili pia ni jukumu letu Wabunge na msisite kutupa kazi ya kuwasiliana au kuwafikia wahusika hawa kama kuna kero za msingi ambazo zinashindwa kutatulika au kuna mizengwe isiyoisha. Moja ya kazi zetu kubwa ambazo ni Mamlaka ya Kikatiba ni kupima na pia kuhoji yanayoendelea ndani ya Serikali-zikiwemo kero mnazozipata. Pale ambapo kuna shukrani kwa wahusika hawa pia tunaweza kuwasaidia kuzifikisha kwa sababu dhumuni la mihimili yote mitatu ya Serikali-Bunge (Parliament), Dola (Executive) na Mahakama (Judiciary) ni kufanya kazi pamoja kama mafiga matatu yanayoshikilia chungu kimoja kinamopikwa chakula ambacho wakusudiwa ni wananchi wanaosubiri wapewe kile kilicho bora. Na maisha bora kwa kila Mtanzania yatakuwa na maana tu kama litakuwa jambo la utekelezaji wa dhati kuona kima Mtanzania, na hasa mwanamke anaishi maisha bora, ana afya nzuri, habaguliwi, hadharauliki, ana nishati na mwanga unaompa nuru ya maisha, ana elimu inayoenda na dunia tunayoishi leo, ana ajira au riziki inayokidhi ugumu wa maisha ya leo, hasumbuki kupatiwa haki anapostahili, anaishi kwa amani na usalama, anapata ujira unaolingana na kazi yake na unaomwezesha kugharimia mambo ya msingi kama pango, nauli, usafiri na kiasi kidogo cha kunywa hata soda, anapata matibabu mazuri anapougua, ana maji safi na salama ya kunywa na matumizi, ana akiba ya uzeeni, na mengi mengineyo.

Nitaendelea.

e-mail: lnyerere@gmail.com